Na K.F.SEMBERA, DAR ES SALAAM
YANGA SC imefanikiwa kwenda hatua ya 16 Bora michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kufuatia kuitoa APR ya Rwanda kwa jumla ya mabao 3-2.
Yanga SC leo imelazimishwa sare ya 1-1 na timu ya jeshi la Rwanda Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam – na kwa kuwa ilishinda 2-1 katika mchezo wa kwanza mjini Kigali wiki iliyopita, inasonga mbele kwa ushindi wa jumla wa 3-2.
Yanga sasa watamenyana na mshindi wa jumla kati ya Al Ahly ya Misri na Recreativo de Libolo ya Angola katika hatua ya 16 Bora.
Katika mchezo wa leo, APR ndiyo waliokuwa wa kwanza kupata bao dakika ya tatu kupitia kwa Fiston Nkinzingabo aliyefumua shuti kali akimalizia pasi ya Jean Claude Iranzi.
Yanga walifanikiwa kusawazisha bao hilo dakika ya 28 kupitia kwa mshambuliaji wake, Donald Dombo Ngoma.
